NYUMBA YA MALEZI MTAKATIFU PLASIDO ABASIA YA PERAMIHO

Nyumba ya malezi ya Mtakatifu Plasido Abasia Peramiho, ni kwa ajili ya waanzaji wa maisha ya kitawa, hasa kwa ajili ya Wakandidati na Wapostulandi.

 
  Kwa nini Mtakatifu Plasido?
Kadiri ya mapokeo yaliyoandikwa na Mtakatifu Gregori , yanasema; Mtakatifu Mauro na Mtakatifu Plasido walikuwa wanafunzi wa kwanza kabisa wa Mtakatifu Benedikto. Maelezo yanasema kwamba tabia zao zilikuwa nzuri sana. Kwa hiyo tumeamua kumchagua mmoja wao kwa lengo la kuwa mfano kwa hao wanaoanza maisha ya kitawa, na pia aweze kuwasindikiza kwa sala na awe msaada pale wanapopambana na mashaka na matatizo katika njia yao ya kutafuta ukamilifu.
KUPOKELEWA KATIKA NYUMBA YA MALEZI YA MTAKATIFU PLASIDO
Vijana wa Kiume wanaojisikia wameitwa na Mungu kuwa Watawa Wabenediktini Wamissionari na wanataka kujiunga na jumuiya ya Abasia ya Peramiho, wanatakiwa kuandika barua ya maombi wakiipeleka kwa Mkurugenzi wa Miito Abasia Peramiho, kupitia Maparoko au Wasaidizi wao. Baada ya barua hizo kumfikia Mkurugenzi wa Miito, yeye atawaalika kuja Peramiho kuona mazingira ya maisha ya kitawa kwa muda wa wiki tatu, kusudi mwombaji ajifunze kutoka kwetu na sisi tujifunze kutoka kwake, kwa kifupi ni kipindi cha kufahamiana. Na hivi mwishoni kila upande uweze kutoa uamuzi unaofaa kwa faida ya sisi sote katika kupata wokovu.
Wale wanaokubaliwa katika nyumba ya malezi wanatakiwa wawe wamefaulu vizuri katika Kidato cha nne na kidato cha sita kuanzia divisheni ya kwanza hadi ya tatu. Aidha, wanakaribishwa wote walio hitimu mafunzo ya Ufundi na wale wa elimu za juu.
 
  MUDA WA MALEZI KATIKA NYUMBA YA MTAKATIFU PLASIDO
Kijana anakaa akilelewa kama Mkandidati katika nyumba ya Mtakatifu Plasido kwa kipindi cha mwaka mmoja, na mwaka unaofuatia atakaa akilelewa kama Mpostulandi tena kwa kipindi cha mwaka mmoja. Katika ujumla wake, kijana anatakiwa kulelewa na kuishi katika nyumba ya malezi ya Mtakatifu Plasido kwa kipindi cha miaka miwili.
NINI KINAFUATA BAADA YA MALEZI KATIKA NYUMBA YA MTAKATIFU PLASIDO?
Baada ya kumaliza kipindi cha malezi katika nyumba ya Mtakatifu Plasido, kijana huyo anategemewa kuyaelewa na kuyafahamu maisha ya kitawa walao tofauti na wakati alipofika kuanza malezi katika nyumba ya Mtakatifu Plasido. Baada ya hapo atapendekezwa kwa ajili ya kupokelewa katika hatua ya UNOVISI, na hapo itampasa kuhama kutoka nyumba ya Mtakatifu Plasido na kuhamia nyumba ya Mtakatifu Benedikto Abasia Peramiho.
 
  Anuani:
Vocation Director
St. Benedict's Abbey
P.O. Peramiho