Nyumbani |
Mahali Maalum
|
Historia |
Schule |
Afya | Yatima | Out Stations |
Musik CD |
Mgusano &
Msaada 
Peramiho Girls Secondary School Historia Kifupi
Kutekeleza azma ya masista ya kumkomboa na kumwendeleza msichana, mwaka 1946 masista walianzisha shule ya wasichana iliyoitwa nyakati zile 'Peramiho Girls' Middle School'. Shule hiyo ilianzishwa na Sr. M. Richardis, OSB, na ilikuwa shule ya kwanza kwa ajili ya wasichana Mkoani Ruvuma.
Kulikuwa na uhusiano baina ya Vyuo vya Maarifa ya Nyumbani na Shule za Msingi ('Middle Schools') za wakati ule ambazo zilianzishwa wakati wa uongozi wa Abate-Askofu Eberhard Spiess, OSB, wa Peramiho. Abate-Askofu alichangia kwa vikubwa mipango ya maendeleo ya elimu ya akina mama. Shule iliyoanzishwa mara ilikua na kusitawi kama mti mchanga katika ardhi yenye rutuba ikisaidiwa kukuzwa na nguvu za masista Wabenediktini.
Pole pole watu walitambua zaidi zaidi na kuona umuhimu wa elimu. Baadaye kulihitajika ziundwe mbinu za kuwaendeleza watu kielimu na kuongeza nafasi za kusoma kwa ajili ya watu wa eneo la kusini mwa Tanzania. Hapo Misioni ya kibenediktini ya Peramiho ilijituma kuanzisha Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkoani Ruvuma.
Mwaka 1968 shule ilisajiliwa kama shule binafsi ya Mapadre Wamisionari Wabenediktini wa Abasia Peramiho. Shule hiyo ilifunguliwa rasmi tarehe 15 Januari 1968 ikiwa na wanafunzi wapatoa 33 wa Kidato cha Kwanza. Mwalimu Mkuu wa kwanza alikuwa Sr. M. Ludovica Koch, OSB, mmisionari kutoka Priorati ya Nebraska huko Marekani. Walimu wengine walikuwa Sr. M. Prisca Komba, OSB, kutoka Chipole, +Sr. M. Cassia Zistler, OSB, na Fr. Bosco Brunner, OSB, aliyekuwa mshauri na mwalimu wa somo la dini.
Baada ya Sr. M. Ludovica kurudi Marekani Sr. M. Elizabeth Sarinas, OSB, alishika nafasi ya uongozi. Walimu wengine toka Ufilipino waliwasili kuongeza nguvu kazi ya shule; nao ni Sr.M. Anselma Paler OSB, Sr. M. Frideswida Ick OSB mwalimu wa somo la Kemia toka Manila. Mwaka 1970 Sr. M. Hereswida Zettler, OSB, alihamishwa Lituhi akaletwa Peramiho kuanzisha somo la fani ya Upishi. Mwaka 1975, chini ya uongozi wa Sr. M. Martina Dreyer, OSB, somo la fani ya Ushonaji lilianzishwa.
Mwanzoni mwa mwezi Mei 1971, Sr. Elizabeth, OSB, alichaguliwa kuwa Mama Mkubwa wa Sjhrika la Masista Wabenediktini wa Majimbo ya Peramiho na Njombe. Naye alimtunuku kazi yake ya uongozi wa shule Sr. M. Bonaventura Kilowoko, OSB, aliyekuwa mwalimu wa Biolojia na Nidhamu.
Mwaka 1995 Wabenediktini wa
Abasia waliwakabidhi rasmi masista Wabenediktini shule ya wasichana
waliyokuwa wameiendesha kwa miaka mingi. Ubadilishaji wa madaraka
ulifanyika wakati wa uongozi wa Mheshimiwa Mama Pia Portmann naye akawa
Meneja mpya wa Shule. Toka
mwaka 1994 shule hiyo ina Vidato vya tano na sita.
