Nini Maana ya Umisionari kwa Siku Hizi ?
"Umisionari" - maana yake nini ? Wengi wanafikiri kuwa umisionari ni kazi ya kuhubiri habari njema kwa watu wasioisikia bado.
Hicho ndicho walichofanya Wabenediktini wa kwanza waliokuja hapa Peramiho mwaka 1898. Leo, mwaka 2009, kazi hii kwa vikubwa imekamilika. Katika eneo waliokabidhiwa mwanzoni, yameundwa majimbo matatu yaani jimbo kuu la Songea, jimbo la Njombe na jimbo la Mbinga. Parokia ya Peramiho yenye wakazi 30,000 ina wakatoliki 20,000.
Jambo hili liliwafanya Wabenediktini wa Peramiho kuanzisha misioni katika sehemu nyingine, yaani kwenye miaka ya 1970 tulianza uinjilishaji nchini Kenya, hasa kwenye Bonde la Kerio. Picha za juu zinatoka Kenya. Siku hizi kanisa mahalia la Kenya limeweza kuendelea na uinjilishaji huo, hivyo sisi Wabenediktini wa Peramiho hatuendelei kuhubiri habari njema kwa watu wasioisikia bado.
Hata hivyo tunajiangalia sisi wenyewe wamisionari Wabenediktini. Kurasa hizi za mtandao zinalenga kukupasha habari za kazi zetu kwa ajili ya utume wa Kanisa.














